Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imefanya Baraza la Wafanyakazi la Sita tarehe 5 na 6 Februari, 2026 katika Manispaa ya Morogoro, kwa lengo la kujadili masuala muhimu ya kiutendaji na maendeleo ya taasisi.
Kikao hicho kiliwakutanisha wajumbe kutoka Menejimenti na Watumishi wa TMDA, ambapo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo kuhusu Mpango Mkakati wa miaka mitano (2026/27–2030/31), Rasimu ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, pamoja na Mpango wa Mazingira, Jamii na Utawala (ESG).
Akihitimisha kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Dkt. Adam Fimbo, amesema ushiriki wa wafanyakazi ni msingi wa mafanikio ya Mamlaka, akisisitiza umuhimu wa uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi.
“Kupitia Baraza hili, tunajenga mshikamano na kuboresha mifumo ya utendaji kwa maslahi ya taasisi na jamii kwa ujumla,” alisema Dkt. Fimbo.
Ameongeza kuwa maoni yaliyotolewa yatazingatiwa katika kupanga na kutekeleza mipango ya TMDA kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma.
Baraza la Wafanyakazi la TMDA hukutana mara mbili kwa mwaka kwa mujibu wa sheria, likilenga kutathmini utendaji, kubaini changamoto, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma.
Kupitia mikutano hiyo, TMDA imeendelea kuimarisha mawasiliano, uwajibikaji na mshikamano kati ya Menejimenti na Watumishi, hali inayochangia utekelezaji bora wa majukumu ya kudhibiti dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine kwa usalama wa afya ya jamii.
TMDA imesisitiza itaendelea kulitumia Baraza la Wafanyakazi kama jukwaa muhimu la kushirikisha watumishi katika maamuzi ya kimkakati na kuendeleza mazingira bora ya kazi.

0 Comments