BMT Kutathmini Utendaji wa Kamati za Michezo Mikoa 12

Katika juhudi za kuimarisha maendeleo ya michezo nchini,Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limepanga kufanya tathmini ya utendaji wa Kamati za Michezo katika mikoa 12 ndani ya robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha.

Lengo la tathmini hiyo ni kuhakikisha kamati hizo zimeundwa kwa mujibu wa sheria na zinafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya BMT.

Kwa mujibu wa BMT, Kamati za Michezo za Mikoa zinajumuisha Afisa Tawala wa Mkoa, Afisa Michezo wa Mkoa, wajumbe walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa, wawakilishi wa vyama vya michezo, pamoja na Maafisa Tawala na Michezo wa Wilaya.

Mkuu wa Kitengo cha Uendelezaji Michezo wa BMT, Benson Chacha, amesema kamati hizo zina jukumu la kusimamia na kuendeleza michezo katika mikoa ikiwemo kukuza vipaji, kuimarisha miundombinu, kusajili vyama na kuratibu mashindano.

Amebainisha kuwa tathmini hiyo itafanyika katika mikoa ya Kagera, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Tabora.

Ameongeza kuwa zoezi hilo pia linalenga kuimarisha mchango wa michezo katika kukuza ajira, mshikamano wa jamii, amani na ushiriki wa wananchi, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya 2050.

Aidha, tathmini hiyo itahusisha ukaguzi wa mifumo ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa vyama na mashirikisho ya michezo ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa misingi ya kitaifa.

Post a Comment

0 Comments