Maseneta wa Marekani Waeleza Wasiwasi kuhusu Mgogoro wa DRC na Hatari ya Njaa

 

Maseneta wa Marekani wameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa migogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hususan maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23, huku wakionya juu ya kuongezeka kwa hatari ya njaa na janga la kibinadamu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wao na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, maseneta hao wamesema hali ya usalama mashariki mwa nchi hiyo inaendelea kuzorota, hali inayochangia mamilioni ya wananchi kukosa chakula na huduma muhimu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa takribani watu milioni 26 wanakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na athari za mapigano yanayoendelea, jambo walilosema halikubaliki na linahitaji hatua za haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Maseneta hao walitoa kauli hiyo kufuatia mkutano uliofanyika nchini Marekani, uliolenga kujadili Makubaliano ya Washington ya Amani na Ustawi pamoja na mustakabali wa ushirikiano kati ya Marekani na DRC.

Kundi la waasi la M23 limeendelea kuwa kiini cha mvutano mashariki mwa DRC, likituhumiwa na Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi kupata msaada kutoka Rwanda, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakana mara kwa mara.

Kwa mujibu wa taarifa, kundi hilo linadhibiti maeneo kadhaa muhimu, ikiwemo miji ya Goma na Bukavu, ambayo liliiteka mwanzoni mwa mwaka 2025.

Kauli ya maseneta Jim Risch (Republican–Idaho) na Jeanne Shaheen (Democrat–New Hampshire), ambao ni viongozi wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Seneti, imekuja saa chache baada ya muungano wa Congo River Alliance, unaojumuisha wapiganaji wa M23, kukiri kuhusika katika shambulio lililotokea wiki iliyopita katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bangoka, mjini Kisangani.

Kuhusu ushirikiano wa DRC na Marekani, maseneta hao wamesisitiza haja ya Rwanda kujiondoa kikamilifu katika maeneo ya mashariki mwa Congo ili kufungua njia ya amani ya kudumu.

Aidha, wamesema Marekani iko tayari kuimarisha ushirikiano wake na DRC, lakini pia iko tayari kuchukua hatua dhidi ya wale watakaokiuka makubaliano ya amani.

Ikumbukwe kuwa Desemba 2025, Rais Tshisekedi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, walisaini makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani, yakilenga kumaliza mapigano mashariki mwa DRC.

Maseneta hao wameeleza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo ni muhimu katika kurejesha utulivu, kulinda raia na kuzuia kuendelea kwa mgogoro wa kibinadamu nchini humo.

Post a Comment

0 Comments