Serikali Yalenga Kuifanya Tanzania Kitovu cha Usafiri na Biashara Afrika

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema mipango inayoandaliwa na Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri, usafirishaji wa bidhaa, viwanda na biashara katika ukanda wa Afrika.

Amesema Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 una dhima ya kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kukuza ukuaji jumuishi na kuongeza ajira, pamoja na kubadili mifumo na mitazamo ya utendaji serikalini.

“Hatua hii itachochea tija katika uzalishaji, kuongeza uwezo wa nchi kushindana kikanda na kimataifa, na kuimarisha muunganiko wa sekta mbalimbali,” amesema.

Dkt. Nchemba alitoa kauli hiyo bungeni leo, Ijumaa Februari 6, 2026, wakati wa hotuba ya kuhitimisha mkutano wa pili wa Bunge, alipokuwa akiwasilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya muda wa kati wa 2026/2027–2028/2029 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027. Bunge limeahirishwa hadi Machi 31, 2026.

Akizungumzia vipaumbele vya matumizi ya Serikali, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kugharimia miradi ya kimkakati inayoendelea, deni la taifa, mishahara ya watumishi wa umma na huduma za jamii.

Ametoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kuweka mkazo katika kusimamia nyongeza ya asilimia tano ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, ili kuimarisha ujasiriamali na ajira.

“Asilimia tano kati ya asilimia 15 ya mikopo hiyo itumike kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji kwa makundi haya,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda wawekezaji wa ndani kwa kuwapa kipaumbele katika zabuni, mikataba na malipo ya madai, pamoja na kuandaa mikakati ya kukuza wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa.

Waziri Mkuu pia amezitaka taasisi na mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara kujitegemea kifedha ifikapo Juni 2029, ili kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Kwa upande wa Serikali za Mitaa, amezitaka kuongeza uwazi katika utekelezaji wa miradi, kuhakikisha taarifa za mapato na matumizi zinawafikia wabunge, madiwani na viongozi husika kwa wakati.

Amesisitiza kuwa gharama na taarifa za miradi zinapaswa kuwa wazi ili kurahisisha ufuatiliaji na kuongeza uwajibikaji.

Ili kuimarisha usimamizi wa miradi, Dkt. Nchemba amewaomba wabunge kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi katika majimbo yao, kushiriki katika uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi, pamoja na kutumia vikao vya ushauri kutoa maoni na ushauri.

Vilevile, amewahimiza viongozi na watendaji wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa mchango wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Sekta binafsi ipewe heshima ili mchango wao uonekane katika maendeleo ya Taifa,” amehitimisha.

Post a Comment

0 Comments