Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea kushuhudiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikieleza kuwa mamilioni ya wananchi wanakabiliwa na changamoto kubwa za maisha.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya OCHA, hali ya kibinadamu nchini humo imefikia viwango vya kutisha, huku zaidi ya watu milioni 5.3 wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro, machafuko na ukosefu wa usalama.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa kufikia mwisho wa mwaka 2025, takribani watu milioni 24.8 hadi 25 walikuwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, hali inayomaanisha kuwa karibu robo ya wananchi wa DRC wanashindwa kupata mahitaji ya msingi ya lishe.
Katika tathmini ya hali ya kibinadamu kuanzia Januari hadi Desemba 2025, OCHA ilibaini zaidi ya matukio 260,500 ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia, mashambulizi dhidi ya raia na ukiukwaji mwingine wa haki za msingi.
Ingawa mgogoro huu umeathiri maeneo mbalimbali ya nchi, mikoa ya mashariki inaendelea kuwa kitovu cha athari kubwa zaidi. Mikoa ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri na Tanganyika imesajili idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani, ikiwa ni sehemu ya watu milioni 5.3 waliokimbia makazi yao.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa makundi yaliyo katika mazingira magumu zaidi, yakiwemo wanawake, watoto na wazee, ndiyo yanayoathirika zaidi na hali hiyo.
“Kaya zilizo hatarini zaidi ndizo waathirika wa kwanza wa mgogoro huu unaozidi kuongezeka,” inaeleza ripoti ya OCHA, ikisisitiza umuhimu wa msaada wa haraka wa kibinadamu.
OCHA imezitaka jumuiya za kimataifa, mashirika ya misaada na wadau wa maendeleo kuongeza juhudi za kutoa msaada wa dharura, ikiwemo chakula, huduma za afya, maji safi na makazi kwa waathirika.
Mgogoro huu unaendelea kuchangiwa na mapigano ya vikundi vya waasi, migogoro ya kisiasa, na changamoto za kiuchumi, hali inayozidi kuhatarisha ustawi wa mamilioni ya raia.

0 Comments