Shirikisho la Soka la Morocco limetangaza nia ya kukata rufaa dhidi ya adhabu ya Dola 715,000 iliyopewa Senegal kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya mataifa hayo mawili.
Katika taarifa iliyotolewa Februari 3, 2026, shirikisho hilo limesema adhabu iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) haitoshi na haifanani na uzito wa vitendo vilivyofanyika wakati wa mchezo huo.
Morocco imesisitiza kuwa itachukua hatua za kisheria kupitia rufaa ili kuhakikisha haki inapatikana na nidhamu inalindwa katika soka la Afrika.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limesema halina mpango wa kukata rufaa dhidi ya adhabu iliyotolewa, likieleza kuwa litawajibika kwa mujibu wa kanuni na taratibu za CAF.
CAF ilitoa adhabu kali kwa timu zote mbili baada ya vurugu na vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyojitokeza wakati wa fainali hiyo.
Kocha Mkuu wa Senegal, Pape Bouna Thiaw, alitozwa faini ya Dola 100,000 baada ya kuwaamuru wachezaji wake kuondoka uwanjani wakati wa mchezo.
Aidha, wachezaji wa Senegal Iliman Cheikh Baroy Ndiaye na Ismaila Sarr walifungiwa kila mmoja kucheza mechi mbili rasmi za CAF kwa kuonesha utovu wa nidhamu kwa mwamuzi.
Shirikisho la Senegal lilitozwa faini ya Dola 300,000 kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki wake, pamoja na faini nyingine ya Dola 300,000 kwa tabia isiyofaa ya wachezaji na benchi la ufundi.
Kwa upande wa Morocco, beki nyota Achraf Hakimi alifungiwa kucheza mechi mbili rasmi za CAF.
Vilevile, Morocco ilitozwa faini ya Dola 200,000 kwa tabia isiyofaa ya wachezaji wake uwanjani, pamoja na Dola 100,000 kwa utovu wa nidhamu wa wachezaji na benchi la ufundi, baada ya kuvamia eneo la ukaguzi wa VAR na kuzuia kazi ya mwamuzi.
CAF imesisitiza kuwa adhabu hizo zinalenga kudhibiti vitendo vya utovu wa nidhamu na kulinda heshima ya mashindano ya soka barani Afrika.

0 Comments