Waandishi wa Habari za Mazingira Wahimizwa Kuandika Habari za Uchunguzi

Katika juhudi za kuimarisha uandishi wa habari za mazingira nchini,waandishi wa habari kutoka Kanda ya Kaskazini na Kati wamehimizwa kujikita katika uandishi wa habari za uchunguzi zitakazosaidia kusukuma mabadiliko ya sera, sheria na kuongeza uwajibikaji katika jamii.

Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari za mazingira yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari Inayosaidia Jamii za Asili (MAIPAC).

Akitoa mada katika mafunzo hayo,Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, amesema kuwa katika uandishi wa kisasa ni muhimu kuandika habari zinazochochea mabadiliko ya sera badala ya kujikita katika taarifa za matukio ya kila siku.

“Mafunzo haya yameandaliwa ili muandike habari za uchunguzi zinazochochea mabadiliko, huku mkizingatia maadili ya taaluma,” amesema Simbaya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MAIPAC,Mussa Juma,amewahimiza waandishi kuzingatia maadili, mila na tamaduni katika uandishi wao, hususan wanaposhughulikia masuala ya jamii za asili.

“Tuandike habari zinazoonesha mapungufu ya sera na sheria, lakini pia zinazoongeza ushiriki wa jamii katika kufanya maamuzi,” amesema Juma.

Akizungumzia uandishi unaohusu jamii za asili,Juma amesema ni muhimu kuheshimu mila na viongozi wa kimila, pamoja na kupata ridhaa ya jamii kabla ya kuandika au kuchapisha taarifa zinazowahusu.

Ameeleza kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kupiga picha na kuandika habari kuhusu jamii za asili bila ridhaa yao, jambo linalokiuka maadili ya uandishi.

Aidha, amewataka wanahabari kuepuka matumizi ya lugha inayodhalilisha au kukera, na kuhakikisha jamii husika zinapewa nafasi ya kujieleza.

Ameongeza kuwa wanatarajia wanahabari kufanya uchunguzi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za pembezoni pamoja na migogoro ya ardhi inayoibuka.

Kwa upande wa masuala ya usalama,Wakili Paul Kisabo aliwataka waandishi kufanya tathmini ya kiusalama kabla ya kwenda kwenye maeneo ya kazi na kuchukua tahadhari stahiki.

Wakili Kisabo pia alieleza umuhimu wa kufahamu na kutumia sheria mbalimbali za habari na mazingira katika utendaji wa kazi za uandishi.

Jumla ya waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Arusha,Kilimanjaro,Tanga,Singida,Dodoma na Manyara walishiriki mafunzo hayo yaliyodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Mafunzo hayo yanatarajiwa pia kufanyika katika Kanda ya Ziwa,Kanda ya Mashariki,Pwani na Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments